Mbunge
wa Hai, Freeman Mbowe akizungumza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa
Wilaya ya Hai, Kilimanjaro jana mara baada ya kulipa faini ya shilingi
milioni moja na kuachiwa huru ,hukumu iliyotokana na kutiwa hatiani kwa
kosa la kumshambulia mwangalizi wa uchaguzi mwaka 2010.
MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amehukumiwa
kulipa faini ya Sh1 milioni au kwenda jela mwaka mmoja baada ya
kupatikana na hatia ya kumshambulia mwangalizi wa Uchaguzi Mkuu mwaka
2010.
Freeman Mbowe.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi wa Wilaya ya Hai, Denis
Mpelembwa. Mbowe, ambaye ni Mbunge wa Hai alilipa faini hiyo
iliyochangwa chapchap na wabunge saba wa Chadema na wafuasi wa chama
hicho waliokuwa mahakamani hapo.
Wabunge waliochanga fedha hizo
ni, Mustafa Akuney wa Mbulu Lucy Owenya, Grace Kiwelu, Cecilia Pareso,
Joyce Mukya, Rose Kalili na Paulin Gekul wote wa Viti Maalumu.
Utata wa kupoteza sifa ya kugombea
Hukumu hiyo iliibua mjadala mkali kwenye mitandao ya kijamii juu ya
uwezekano wa kumzuia Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Upinzani Bungeni
kuwania tena ubunge au urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba.
Hata
hivyo, Mwanasheria, Alex Mgongolwa akinukuu Katiba ya Tanzania Ibara ya
67 (1)(c); 67(2) (c na d) alisema hukumu hiyo haiwezi kumzuia kugombea
ubunge kwa sababu hakwenda jela na kosa lake halihusu kukosa utovu wa
uaminifu, kukwepa kodi wala kuvunja Sheria ya Maadili ya Viongozi wa
Umma.
Suala hilo linafanana na lililotokea katika mchakato wa
uteuzi wa wagombea urais mwaka 2005 wakati aliyekuwa mgombea urais wa
DP, Mchungaji Christopher Mtikila na mgombea mwenza wake, Saidi Soud
Said walipowekewa pingamizi kutokana na kutumikia kifungo jela, Mtikila
akitumikia mwaka mmoja kwa kosa la uchochezi, Said akitumikia chuo cha
mafunzo kwa kosa la biashara ya vitambaa. Hata hivyo, pingamizi hilo
lilitupwa na aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
Jaji Lewis Makame (marehemu) baada ya kusikiliza utetezi wa Mtikila na
Said, kuwa makosa waliyofungwa kwayo hayakuwa ya kukwepa kodi, kukosa
uaminifu wala kukiuka maadili ya viongozi wa umma.
MashtakaMbowe
alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya kumfanyia shambulio la kawaida,
mwangalizi wa ndani wa Uchaguzi Mkuu Oktoba 31, 2010, Nassir Yamin
katika kituo cha kupigia kura kilichokuwa katika Zahanati ya Lambo.
Yamin alikuwa ni mwangalizi wa kutoka Baraza Kuu la Waislamu wa Tanzania (Bakwata).
Akitoa
hukumu hiyo, Hakimu Mpelembwa ambaye amehamishiwa Bukoba, alisema
kitendo kilichofanywa na Mbowe hakikubaliki na kinapaswa kukemewa.
“Kitendo
alichokifanya mshtakiwa akiwa Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema na Mbunge
wa Jimbo la Hai ambaye alipaswa kuwa kioo cha jamii hakikubaliki na
lazima kikemewe,” alisema.
“Kwa hiyo hukumu ya Mahakama ni kwamba
atalipa faini ya Sh1,000,000 au akishindwa kulipa atakwenda magereza kwa
mwaka mmoja,” alisema hakimu huyo.
UshahidiAkichambua
ushahidi uliomtia Mbowe hatiani, Hakimu huyo alisema Mahakama imeegemea
ushahidi wa shahidi wa kwanza, Yamin na shahidi wa pili John Mushi
aliyekuwa msimamizi wa kituo.
Alisema ushahidi huo ulieleza kuwa
siku hiyo Mbowe aliingia katika Kituo cha Zahanati ya Lambo katika Jimbo
la Hai na kuuliza uhalali wa mlalamikaji kuwapo kituoni hapo.
Mashahidi
hao waliiambia Mahakama kuwa walimuona Mbowe akimkunja na kumtoa nje
kwa nguvu mwangalizi huyo wa ndani na baadaye mbunge huyo kuondoka
katika kituo hicho.
Alisema ushahidi wa mashahidi hao uliungwa
mkono na shahidi wa nne wa mashtaka, ambaye ni daktari wa Hospitali ya
Wilaya ya Hai, aliyemtibu mlalamikaji na kujaza fomu PF3.
Alisema
ushahidi wa daktari huyo unaonyesha kuwa mlalamikaji alikuwa na
michubuko katika shavu lake moja na shingoni iliyotokana na kupigwa na
kitu butu.
Hata hivyo, aliukataa ushahidi wa shahidi wa saba,
Mkaguzi Msaidizi wa Polisi, Shafii aliyekuwa mpelelezi mkuu kuwa Mbowe
alikiri kufanya kosa hilo alipoandika maelezo ya onyo polisi.
Hakimu
Mpelembwa alisema japokuwa upande wa mashtaka uliwasilisha maelezo hayo
kama kielelezo lakini baada ya kuyapitia, hakuna mahali ambako Mbowe
alikiri kufanya kosa hilo.
Utetezi wa MboweHakimu
Mpelembwa alisema wakati akijitetea mahakamani, Mbowe alikanusha
kufanya tukio hilo lakini alikiri kufika katika kituo hicho na kumtaka
mwangalizi huyo kumwonyesha kitambulisho chake.
“Katika utetezi
wake, mshtakiwa alikanusha kumpiga Nasir Yamin wala kumfanyia kitu
chochote kibaya, bali alimwamuru atoke nje kwani hakuwamo kwenye orodha
ya waangalizi iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”
Hakimu
huyo alisema, Mbowe alieleza kuwa hakuwahi kuitwa polisi, bali alikwenda
mwenyewe baada ya kusikia kwenye vyombo vya habari kuwa amefunguliwa
kesi ya aina hiyo.
Sababu za kutiwa hatianiHakimu
Mpelembwa alifafanua dhana ya kosa la shambulio kuwa ni kitendo
chochote chenye nia ya kudhuru mtu mwingine au hata kujaribu tu kumdhuru
au kumtia hofu.
“Kwa maana nyingine ni kitendo cha kumtia mtu
mwingine hofu na ili kosa hilo litimie ni lazima mshtakiwa awe na nia
isiyo halali kisheria ya kutaka kutenda kosa nililolianisha,” alisema.
Hata
hivyo, hakimu huyo alisema shahidi wa kwanza (Yamin) na wa Pili
(msimamizi) waliiambia Mahakama kuwa mshtakiwa alimkunja na kumvuta nje
mlalamikaji atoke nje ya kituo.
“Ushahidi wa Yamin na Mushi ni wa
kuona kuwa mshtakiwa alimkunja na kumtoa nje mlalamikaji. Swali hapa ni
je, kumvuta mtu na kumtoa nje kunapelekea kosa la shambulio?” alihoji.
Hakimu
huyo alisema kwa tafsiri ya dhana nzima ya kosa la shambulio ni dhahiri
kitendo alichokifanya mshtakiwa kinaangukia katika kosa hilo kwa mujibu
wa sheria.
“Ushahidi wa shahidi wa kwanza na wa pili wa upande
wa mashtaka unashabihiana na ushahidi wa daktari kwamba kulikuwa na
michubuko. Kwa mantiki hiyo Mahakama inakubali ushahidi huo. Kutokana na
Mahakama kukubali ushahidi wa mashahidi hao watatu, inakutia hatiani
kwa kosa la shambulio kama ulivyoshtakiwa nalo.”
Mwendesha
mashtaka, Inspekta Msaidizi wa Polisi, Feo Simon alisema ingawa hawana
kumbukumbu ya makosa ya nyuma ya mshtakiwa, aliiomba itoe adhabu kali
ili iwe fundisho kwake na kwa jamii.
Wakili wa Mbowe, Issa Rajabu
aliyekuwa akisaidiana na Albert Msando, aliomba Mahakama impe adhabu
ndogo mteja wake kwani hajawahi kutenda kosa lolote la jinai.
Hata
hivyo, Hakimu Mpelembwa alisema kwa kutoa adhabu ya faini ya Sh1
milioni au kifungo cha mwaka mmoja jela amezingatia ombi la wakili wa
Mbowe.
Baada ya hukumuHukumu hiyo iliyoanza
saa sita mchana hadi saa 7.20 mchana, wafuasi wa Chadema waliokuwa
wamefurika mahakamani hapo walitandika kanga chini na kuanza
kuchangishana faini hiyo kazi ambayo ilisimamiwa na Kiwelu.
Wakati
kazi hiyo ikiendelea, Mbowe aliendelea kushikiliwa ndani ya chumba cha
Mahakama hadi wabunge hao walipokwenda Benki ya NMB, Tawi la Hai saa
7.40 mchana na kulipa faini hiyo na Mbowe kuachiwa saa nane mchana.
Mbowe azungumzia hukumuAkizungumza
nje ya chumba cha Mahakama hiyo, Mbowe aliwatoa hofu wanachama wa
Chadema kwamba wasikatishwe tamaa na hukumu hiyo ambayo alisema
alitegemea ingekuwa hivyo.
“Mnanipa pole ya nini? Kuna msiba
hapa? Tupeane hongera. Sikutarajia cha tofauti na hiki kilichofanyika.
Hakinivunji nguvu, bali kinaniimarisha katika mapambano,” alisema.
“Haki
katika nchi hii itapiganiwa kwa watu wengine kuumia na wengine kuokoka.
Nimesota mahakamani miaka mitano badala ya kufanya kazi ya wananchi.
Hainivunji moyo,” alisema na kuongeza:
“Hainivunji moyo katika
azma yangu ya kuikomboa nchi hii na ukombozi uko jirani. Mahakama ya
nchi hii vimekuwa ni vyombo vya kutoa dhuluma kwa wananchi japo siyo
mahakimu wote. Lakini iko siku Mahakama zitakuwa ni sehemu ya kutolea
haki, kutenda haki na haki ionekane imetendeka. Mapambano yanaendelea na
nawaomba msiwe wanyonge,” alisisitiza.
“Sitaki kuizungumzia
Mahakama katika hatua ya sasa lakini ndani ya Mahakama kuna watu
wanaotenda haki na ndani ya Mahakama kuna watu wasiotenda haki,” alisema
Mbowe.
Alisema kesi hiyo haikustahili kuiendesha kwa miaka
mitano na kwamba kodi za wananchi zinateketea pamoja na muda, akisema
haiwezekani nchi ikaendeshwa katika utaratibu huo.
“Kama mimi
mbunge, Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, mtunga sheria wa
nchi hii naweza kusoteshwa mahakamani miaka mitano, mwananchi wa kawaida
atafanywaje?” alihoji Mbowe.
(CHANZO: GAZETI LA MWANANCHI, ALHAMISI, JUNI18 2015)