Stori: Hamida Hassan na Imelda Mtema HALI bado tete!
Siku chache baada ya Mwenyekiti wa Klabu ya Bongo Movie Unity, Steven
Mengere ‘Steve Nyerere’ kujiuzulu, upepo mbaya unaendelea kuitafuna
klabu hiyo ambapo sasa wasanii wengine watano wamejiengua, Risasi
Mchanganyiko linakupa mchapo kamili.
Msanii wa filamu Bongo, Halima Yahya ‘Davina’.
Kutokana na wasanii hao kujitoa, klabu hiyo inaonekana kupoteza
muelekeo ambapo kwa sasa wanachama waliobaki kundini wanajipanga upya
ili kuisimamisha upya.
Kwa mujibu wa chanzo makini, wasanii
waliojiengua ni Halima Yahya ‘Davina’, Esha Buheti, Kajala Masanja,
Flora Mvungi na Salma Salmini ‘Sandra’ huku sababu kubwa ikitajwa kuwa
ni kukithiri kwa vitendo vya ngono na ubaguzi wa kimaslahi.
Msanii wa filamu Bongo, Flora Mvungi akipozi.
Chanzo hicho kilizidi kumwaga ubuyu kwamba, hivi karibuni kulitokea
safari ya wasanii kwenda mkoani Tanga lakini baadhi ya viongozi
wamedaiwa kujichagua kwa ‘kapo’ bila kujali kuwa wapo wanachama wengine
ambao wanatakiwa kwenda huko.
Kikifafanua madai hayo, chanzo hicho kilikwenda mbele zaidi na kuzinadi kapo hizo kama ifuatavyo:
Cloud 112 (Issa Musa) alidaiwa kuongozana na Coletha Raymond, JB (Jacob
Steven) na Shamsa Ford, Rose Ndauka na Single Mtambalike (Rich) na
wengine.
Msanii wa filamu Bongo, Kajala Masanja.
Baada ya madai hayo kutua kwa mapaparazi wetu, walianza kwa
kuwatafuta walengwa ambao wamedaiwa kubaguliwa na kuamua kujitoa klabuni
hapo. Mambo yalikuwa hivi:
Davina: “Mimi nimeamua kujitoa kwa sababu naona
mambo mazuri wanachaguana mapatna tu sisi tunakumbukwa pasipo mazuri,
kwenye pesa wanapeana wao wenyewe, mimi mpaka mume wangu alikuwa
akiniuliza kwamba napata faida gani.”
Msanii wa filamu Bongo, Salma Salmini ‘Sandra’
Sandra:
“Sijapata faida yoyote Bongo Movie, watu wanapeana mapatna inapotokea suala la safari na pesa.”
Esha Buheti: “Mimi nimeamua kujitoa kwani watu
wamekuwa na ubaguzi, sisi tunaitwa unapotokea msiba tu, nitafanya kazi
zangu mdogomdogo, nitatoka tu.”
Msanii wa filamu Bongo, Esha Buheti.
Kajala: “Nimejitoa kwa sababu kule nilikuwa nikimfuata Steve Nyerere, sasa ameshatoka nafuata nini tena?”
Jitihada za kuwapata wasanii wanaotajwa kuwa ni wabaguzi ziligonga
mwamba kwa baadhi ya wasanii lakini alipopatikana Cloud 112, alikanusha
taarifa hizo.
“Hakuna kitu kama hicho, sisi tunasafiri kulingana na matakwa ya
waandaaji wa safari, waandaaji ndiyo wanaosema wanamtaka nani katika
shughuli yao, wanaosema hivyo wamekosa la kuongea,” alisema Cloud 112.