Katibu
Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani, Mbarak Abdulwakil akizungumza jana
kuhusu kufutwa kwa ajira 200 Uhamiaji. Kulia ni Mkurugenzi wa Upelelezi
wa Makosa ya jinai nchini (DCI), Isaya Mngulu. Picha na Venance Nestory
Wizara
ya Mambo ya Ndani imefuta ajira 200 za konstebo na koplo katika Idara
ya Uhamiaji baada ya kubaini kuwa kulikuwa na upendeleo katika usaili na
sasa zitatangazwa upya na kusimamiwa na wizara hiyo.
Akizungumza
Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mbarak Abdulwakil
alisema hatua hiyo imechukuliwa baada ya kamati maalumu ya kuchunguza
ajira hizo kubaini wazi kwamba waliopewa nafasi hizo hawakukidhi vigezo.
Abdulwakil
alisema wizara imesikitishwa na udhaifu huo baada ya kubainika wazi
kwamba malalamiko yaliyotolewa na wananchi na kusababisha wizara
kuingilia kati na kufuta usaili wa kuitwa kwenye ajira kwa watu 200
ulikuwa sahihi.
Alisema
baada ya kubainika kwamba kweli kulikuwa na upendeleo wa dhahiri kwani
watahiniwa wenye sifa na waliopata alama za juu wakati wa usaili
hawakuitwa na kukiukwa kwa vigezo vya wazi, ajira hizo zitatangazwa upya
na kusimamiwa moja kwa moja na wizara na siyo idara hiyo kama
ilivyokuwa awali.
“Kamati
hiyo iliyoanza kazi yake Agosti Mosi, mwaka huu ilibaini kwamba hata
kigezo cha umri, ambacho ni miaka 25 kwa konstebo na miaka 30 kwa koplo
hakikuzingatiwa kwani wenye umri zaidi ya huo waliitwa kazini... “Lakini
zaidi, baadhi ya wasailiwa walioitwa kazini ni ndugu na jamaa wa
watumishi wa Idara ya Uhamiaji,” alisema.
Alieleza
kwamba utaratibu mpya wa kuwapata watu wanaostahili utatangazwa kupitia
vyombo vya habari na mamlaka ya usimamizi imerejeshwa kwenye wizara
husika badala ya kuachiwa kwenye idara husika.
Alisema
pamoja na kwamba miongoni mwa udhaifu uliobainika ni kwamba matangazo
ya kazi yaliyotolewa kwenye vyombo vya habari hayakuainisha viwango na
madaraja ya ufaulu kwa waliomaliza kidato cha nne na cha sita, lakini
hata wale waliofanya vizuri katika usaili hawakuitwa kazini na hakuna
sababu maalumu zilizotolewa.
Alisema ajira hizo zilizofutwa zinahusisha pia nafasi 28 zilizokuwa zimetangazwa kupitia Idara ya Uhamiaji Zanzibar.
Alisema
si kosa kwa ndugu na jamaa wa watumishi wa Idara ya Uhamiaji kuajiriwa
katika nafasi hizo iwapo wanakidhi vigezo vyote, lakini inapotokea
kwamba hakuna msimamizi huru ni wazi kwamba kunakuwa na upendeleo kama
ilivyotokea na idara hiyo haichukui watumishi kutoka Sekretarieti ya
Ajira, kwa kuwa wanaohitajika ni askari.
Ajira
hizo zilitangazwa Februari 17, mwaka huu na watu 15,707 walijitokeza
kuwania nafasi hizo 200, miongoni mwao, waombaji 1,005 waliitwa kwenye
usaili na 200 waliothibitishwa waliitwa kazini.
Hata
hivyo, baada ya tangazo la kuitwa kazini malalamiko yaliibuka kupitia
vyombo vya habari na baadhi ya mitandao ya kijamii, kwamba baadhi ya
walioitwa katika ajira hizo walikuwa ni watoto, jamaa na ndugu wa
maofisa wa Idara ya Uhamiaji.
Baada
ya kuibuka kwa malalamiko hayo, wizara iliingilia kati na kuunda kamati
hiyo ya watu watano Julai 31, ambayo ilipewa siku 10 kukamilisha kazi
yake na kutoa matokeo.