Nianze
kwa kumshukuru Maulana kwa kutuwezesha kuiona salama siku ya leo, ni
matumaini yangu kwamba msomaji wangu uko vizuri na unaendelea
kulisongesha mbele gurudumu la maendeleo.
Wiki iliyopita tulianza
kujadili mada juu ya umuhimu wa kutoka ‘out’ na umpendaye. Tuliona jinsi
kutoana out kunavyoweza kufufua mapenzi kati ya wawili wapendao bila
kujali wameishi kwa muda gani katika uhusiano wa kimapenzi.
Tuendelee
na sehemu ya pili ya mada yetu ambapo tutazungumzia mambo ya muhimu ya
kuzingatia mnapotoka ‘out’ na yale ambayo hutakiwi kabisa kuyafanya
unapotoka na umpendaye.
1. MAANDALIZI
Unapopanga
kutoka na umpendaye, ni vizuri kufanya maandalizi ya kutosha ya vitu
vyote muhimu ili siku ikifika, isionekane umekurupuka. Ni vizuri kufanya
maandalizi ya sehemu unayotaka kumpeleka mwenzi wako na kuhakikisha ina
utulivu wa kutosha na usalama.
Baada
ya kuwa na uhakika na sehemu mtakayoenda, ni vizuri kujiandaa wewe
binafsi. Andaa nguo safi, fanya usafi wa mwili ikiwa ni pamoja na kuoga
vizuri na kupiga mswaki kwani mkiwa out, lazima mtasogeleana na mwenzi
wako hivyo kama unanuka mdomo au jasho, unaweza kuwa kikwazo kwa mwenzi
wako.
Hata kama hatakwambia, hatafurahia kuwa na wewe karibu. Unaweza pia kujipulizia marashi mazuri yatakayoongeza bashasha.
2. MPE KIPAUMBELE
Baada
ya maandalizi ya awali kuwa yamekamilika, jitahidi kuwahi kabla ya muda
mliokubaliana. Akifika na kukukuta tayari umeshafika na kumsubiri,
ataona umempa kipaumbele, jambo litakalomfurahisha. Mpokee kwa
uchangamfu, inuka, muoneshe sehemu ya kukaa na akishakaa na kutulia, na
wewe kaa kisha muulize kitu atakachokipendelea.
Anzisha
mazungumzo ya kawaida huku ukijitahidi kuwa na tabasamu kwenye uso wako
kwani kuna usemi wa wahenga kwamba tabasamu ni kama uchawi wa
kimapenzi, hata kama mwenzi wako ana hofu ndani ya moyo wake, akikuona
umetabasamu, atatulia na kufurahia kuwa pamoja na wewe.
3. EPUKA MATUMIZI YA SIMU
Watu
wengi huwa wanakosea jambo moja, unakuta bibi na bwana wametoka ‘out’
lakini kila mmoja yuko bize na simu yake. Mwanaume yuko bize kuchat
Whatsapp au Facebook, mwanamke yuko bize Instagram au kutuma meseji za
kawaida.
Nakushauri
msomaji wangu usiwe na tabia kama hii kwani haileti picha nzuri.
Ikiwezekana, zima kabisa simu yako au itoe mlio ili akili yako yote
uielekeze kwa mwenzi wako. Utajisikiaje pale unapomwambia mwenzio kitu
kizuri lakini kumbe wala hakusikilizi yuko bize na simu yake? Haileti
picha nzuri.
4. EPUKA MATUMIZI YA POMBE KUPITA KIASI
Kama
wewe ni mtumiaji wa kilevi, jizuie kunywa hadi kulewa wakati ukiwa
kwenye mtoko na mwenzi wako. Kwa kawaida, mtu aliyelewa, hawezi
kuzungumza kwa busara, anaweza kufanya jambo lolote la aibu bila kujijua
na hawezi kuwa makini katika mazungumzo. Epuka kulewa ukiwa out na
mwenzi wako.
5. ZUNGUMZA KWA BUSARA
Badala
ya wewe kuwa mzungumzaji mkuu, washauri wa mambo ya mapenzi wanaeleza
kwamba ni lazima uongozwe na busara katika kila unachokizungumza. Achana
na habari za wapenzi wako waliopita, zungumza naye mambo mazuri ikiwemo
mipango ya maisha ya baadaye na jitahidi kuwa msikilizaji kuliko
mzungumzaji.
Ni
matumaini yangu kwamba ukizingatia haya, utafanikiwa ‘kumroga’ mpenzi
wako, ataendelea kukupenda na muda mwingi atakuwa akikufikiria wewe
pamoja na kukumbuka mambo mazuri mliyoyafanya pamoja mkiwa out.