Ndugu
zangu, maisha ya kimapenzi yanahitaji uvumilivu wa hali ya juu sana
kwani kuna changamoto nyingi zinazoweza kujitokeza kiasi kwamba
usipoangalia unaweza kuishia kusema hutakuja kumpenda mtu, heri uishi
peke yako!
Tatizo
kubwa ambalo limekuwa likiwasumbua wengi walio kwenye ndoa na wale
walio kwenye uhusiano wa kawaida ni usaliti. Uaminifu umepungua kwa
kiasi kikubwa, mke wa mtu kutembea na rafiki wa mumewe si kitu cha ajabu
siku hizi, mume wa mtu kutembea na mpangaji mwenzake siyo ishu.
Lakini
katika uchunguzi uliofanywa imebainika kuwa baadhi ya wake za watu
wamekuwa wakitengeneza mazingira ya waume zao kutembea na marafiki
/mashosti zao.
Unaweza kushituka kusikia hivyo lakini ndiyo ukweli wenyewe na utakubaliana na mimi baada ya kusoma vipengele vifuatavyo.
1. Ukaribu wa mume na marafiki wa mke
Kuna
baadhi ya wanawake wamekuwa na tabia ya kuwaweka waume zao karibu sana
na marafiki zao. Unakuta mwanamke eti anamruhusu mumewe kwenda klabu au
baa na shosti wake. Katika mazingira hayo unatarajia nini?
Sisemi
uanze kumfikiria tofauti rafiki yako lakini unachotakiwa kujua ni
kwamba, sasa hivi kuna wasichana micharuko ambao ukiwapa nafasi kidogo
tu kwa mumeo wanakupindua.
Kwa
maana hiyo kitendo cha kumuweka mumeo karibu na mashosti wako
unatengeneza mazingira ya kusalitiwa kwa kujitakia hivyo unatakiwa kuwa
makini na watu ambao wanastahili kuwa karibu na laazizi wako.
Mawasiliano ya mume na marafiki wa mke
Sisemi
marafiki zako wasiwasiliane kabisa na mumeo lakini unatakiwa kuangalia
wanawasiliana kwa mambo gani? Utakuwa ni mtu wa ajabu kama utakubali
mumeo apigiwe simu au achati na marafiki zako halafu hakuna cha maana
wanachoongea, walahi utaula wa chuya!
Unatakiwa
kuwa mkali pale unapoona mumeo anawasiliana sana na marafiki zako wa
kike kwani waliosalitiwa walianza kuchukulia poa mazingira kama hayo
mwishowe wakalia.
2. Mke kuanika siri za mumewe
Lingine
ni tabia ya baadhi ya wanawake kuwasimulia mashosti wao siri ambazo
hawastahili kuzitoa nje. Kuna wanawake sijui nisema ni ulimbukeni au
ushamba!
Eti
unamkuta mke anasimulia mashosti wake jinsi mumewe anavyompa furaha
wanapokuwa faragha. Unajiuliza ni kwa nini mtu anafikia hatua hiyo.
Kimsingi
hili ni kosa kubwa linalofanywa na baadhi ya wanawake na kujikuta
wakikaribisha usumbufu kwa waume zao kutoka kwa wanawake micharuko.
3. Mwanamke kutochukua nafasi yake
Kwa kifupi mwanamke kushindwa kumdatisha mumewe ni kumfanya aangalie wapi kwingine anakoweza kupatiwa kile anachokihitaji.
Hili
liwe fundisho kwa wanawake waliobahatika kuingia kwenye maisha ya ndoa.
Kumridhisha mumeo ni kumfanya aepukane na vishawishi vinavyoweza
kumfanya akusaliti.
Mpe
mapenzi atosheke asifikiria kukusaliti, mpe kila anachokitaka kutoka
kwako (ila usimruhusu kuruka ukuta). Hii itamfanya asiwe na tamaa ya
kupoteza muda wake kwa marafiki zako ambao ni micharuko wanaotamani
kuonja asali yako.