NDUGU
zangu, mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha yetu ya kila
siku. Hakuna anayeweza kusimama na kusema, hataki kujihusisha nayo kwa
namna yoyote, akijitokeza huyo atakuwa na matatizo ya akili.
Mimi
na wewe tunahitaji kuwa na wapenzi tena wenye mapenzi ya dhati ili
maisha yetu yaweze kukamilika. Bila kuwa na mtu ambaye kuna wakati
unammisi, lazima utahisi kupungukiwa kitu fulani muhimu katika maisha
yako.
Lakini
wakati ukweli ukiwa hivyo, wapo wanaochukulia mapenzi kama kitu
rahisirahisi. Kitu ambacho anaweza kuingiza usanii na mambo yakaenda.
Hapa
namaanisha hivi, mtaani kuna watu wa aina mbili. Kuna ambao wanajua
kweli kupenda. Akisema anampenda fulani, anamaanisha na hata ukimpasua
moyoni mwake utakuta mtu huyo amechukua nafasi kubwa sana.
Lakini
kuna wale ambao wanaweza kusema wamependa kumbe wametamani au wana nia
zao wanazozijua wenyewe. Unamkuta mwanaume anadanganya kuwa ametokea
kumpenda msichana fulani na ana dhamira ya kufunga naye ndoa lakini
kumbe hana lolote, nia yake amuonje kisha aingie mitini.
Achilia
mbali hao, kuna wanaume ambao wanatumia pesa na utaalam wao wa kuongea
kuwarubuni wasichana ili watembee nao kwa kipindi fulani kisha
wakisharidhika, wanawaacha. Wavulana hao wapo na wamekuwa ni tatizo
kubwa huko mtaani.
Lakini
pia wapo wasichana ambao wenyewe wanajiita wa mjini. Yaani wao hawajui
kupenda, wanachoangalia ni mwanaume ‘mwenye nazo’. Wakishampata,
watajifanyisha kuwa na mapenzi ya dhati kupita maelezo. Maneno kama
dear, honey, sweet na mengineyo matamu yatatawala midomoni mwao lakini
kumbe wizi mtupu.
Katika
mazingira hayo sasa utaona ni kwa jinsi gani mapenzi yamekuwa janga.
Ndiyo maana leo hii wapo wanaotamani kutojihusisha na mambo ya mapenzi
kwa sababu hizihizi za usanii na ujanjaujanja mwingi.
Wakati
mambo yakiwa hivyo, kuna baadhi ya watu ambao wamekithiri kwa tabia ya
kuwatesa wapenzi wao kisa wameoneshwa kuwa wanapendwa sana. Naandika
haya nikiwa na malalamiko ya wasomaji wangu wengi wakieleza namna ambayo
kupenda kwao kunawatokea puani.
Wapo
watu ambao wakipenda wamependa kweli na hawawezi kujizuia kuonesha
hisia zao kwamba ‘wamekufa’. Hatua hiyo sasa hivi badala ya kuwa
changamoto kwa aliyependwa ili naye aongeze mapenzi, inakuwa tatizo.
Uchunguzi
unaonesha kuwa, sasa hivi mwanaume akioneshwa kupendwa sana na
mwanamke, atavimba kichwa na kumfanyia mwenzake kila aina ya visa eti
kwa kuwa amebaini amependwa na hawezi kuachwa.
Hili
halipo kwa wanaume tu. Wapo wanawake ambao nao kwa kujua kuwa waume zao
wamekufa kwao, dharau inaongezeka, heshima inapungua na kufanya hata
yale ambayo wanajua yanawakera wenzao.
Hivi
kwa nini tufikie hatua ya kuwatesa watu ambao wameshindwa kujizuia
kuonesha mapenzi yao kwetu? Kupendwa sana imekuwa nongwa jamani? Hujui
kwamba kupendwa ni bahati?
Mbaya zaidi mtu anakutamkia kwamba anakupenda sana na wewe unajibu kuwa nawe unampenda, kumbe hamna lolote.
Matokeo
yake sasa kadiri siku zinavyokwenda, unaanza kuonesha uhalisia kwamba
humpendi kwa matendo. Hii siyo sawa. Mimi nadhani kama humpendi mtu ni
vyema ukamwambia mapema ili asikupe nafasi kwenye moyo wake.
Unapokubali
kuwa na wewe unampenda kisha baadaye unaanza kumtesa kwa kumfanyia
mambo ambayo hakuyatarajia, unafanya makosa na ni dhambi hata kwa Mungu.
Kama
kweli unapenda, mdhihirishie kwa matendo ili asiwe na shaka kwamba
huenda ameingia kwenye penzi la kisanii, lakini kama yeye amekutamkia
kuwa anakupenda lakini wewe ukahisi huna mapenzi naye, kuwa muwazi kwake
ili ajue wazi amempenda mtu ambaye hampendi!