Umeshawahi
kujiuliza unaweza kuufanyia nini mshahara wa shilingi elfu 60 kwa
mwezi? Basi usishangae pale unapozidishiwa bili, unapoombwa ofa au
kutegwa kwa namna yoyote ili utoe fedha zaidi, hii yote huja ili
kuongezea kipato.
Piga
hesabu hizi, kodi ya chumba shilingi 15,000, nauli ya daladala kwa siku
tufanye shilingi 800 kwa siku (inaweza kuwa zaidi kwa wanaopanda mabasi
manne kwa siku) , kilo moja ya unga 900, sukari shilingi 2,000 ukipiga
na mahitaji mengine muhimu unaweza kuona hii shilingi elfu 60 inaisha
ndani ya siku mbili tu.
Sasa
je wanamudu vipi gharama za maisha ambazo zinapanda kila kukicha? Salma
Chitenga (Sio jina lake halisi) anasema kila kazi ina mbinu zake; kwani
kila mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake.
Anasema
yeye na wenzake sita wanaishi katika chumba walichopewa na mmiliki wa
baa anayoifanyia kazi iliyopo maeneo ya External jijini Dar es Salaam.
“Ninaishi
katika chumba tulichopewa na mmiliki wa baa ninayoifanyia kazi (
mwenyewe analiita ‘ghetto’) akisema kuwa fedha anazolipwa zinamsaidia
kujikimu na kusaidia ndugu zake waliopo kijijini.
“Ninalipwa
shilingi 60,000 kwa mwezi, lakini kila siku ninapewa shilingi 1,500 kwa
ajili ya chakula, pia tajiri ametupa chumba tunaishi hapa, fedha
ninayopata ninanunua nguo na pia kiasi kidogo huwa ninamtumia mama yangu
kijijini,” anasema Salma.
Aisha
Suleiman ni mfanyakazi wa baa na ni mama wa mtoto mmoja wa kiume mwenye
umri wa mwaka mmoja na nusu. Yeye anasema changamoto yake kubwa iliyo
mbele yake ni jinsi ya kuibana fedha ndogo anayoipata.
“Nina
mtoto mdogo ambaye anahitaji matunzo na mshahara wenyewe ni duni,
inabidi nitumie mbinu mbalimbali kujiongezea kipato,” anasema Aisha.
Aisha
anasema zipo njia nyingi za kujiongezea kipato ambazo wafanyakazi wa
baa huzitumia huku akisisitiza kuwa zipo mbaya na nzuri.
Anakiri
kuwa mshahara wa shilingi 60,000 ni mdogo hasa kwa mtu mwenye familia
kama yeye kwani lazima apange chumba na aache hela ya chakula kila siku.
“Kwa
kuwa kazi zangu ninafanya usiku, inabidi katika hiyo fedha ninunue na
maziwa ya mtoto pia nimuachie fedha kidogo mtu anayenitunzia mtoto wangu
wakati sipo, nimeshindwa kuajiri mfanyakazi wa ndani kwa kuwa kipato
changu ni kidogo,” anasema Aisha.
Waswahili
wanasema njaa huleta akili na hivi ndivyo anavyosimulia Aisha akisema
kuwa msukumo wa kutafuta fedha zaidi umetokana na majukumu aliyonayo kwa
familia yake “Kuna njia nyingi za
kujiongezea kipato, mfano ukipata wateja na kuwapa huduma nzuri hawawezi
kuondoka bila kukupa chochote au hata ofa ya kinywaji,” anasema na
kuongeza.
“Ukiwa
mkarimu kwa mteja, hasa wanaume, anaweza kukupa ofa ya bia, hapo ni
ujanja wako sasa ‘kucheza’ ili ile ofa usiinywe na badala yake uchukue
fedha kwasababu wateja wengine akikupa bia anakulazimisha uinywe,”
anasema Aisha.
Aidha
anasema hategemei ofa za bia peke yake, anapohudumia wateja vizuri pia
humpa kitu kidogo maarufu kwa jina la ‘tip’ akisema hizo pekee kwa siku
kama mambo yakienda vizuri anaweza kupata hata Sh 5,000.
Hii
ni sehemu tu ya maisha ya wafanyakazi wa baa, wapo ambao hulipwa
kutokana na huduma waliyotoa kwa siku, wapo ambao hulipwa kwa kuongeza
bei ya kawaida ya vinywaji ya baa husika, lakini wapo ambao hujilipa
wanavyojua wenyewe.