KATIKA hali
ambayo siyo ya kawaida iliyowashangaza wakazi wa eneo la Ukonga
Mazizini kwa Makobe, baba mmoja aliyefahamika kwa jina la Elisha Zakari
amedaiwa kumpiga mwanaye wa kumzaa kipigo kama cha ng’ombe machungani
na kusababishaazimie na kulazwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
Mtoto Amani Elisha (10) aliyepigwa vibaya na baba yake mzazi hadi kuzimia kwa siku mbili.
Mtoto
huyo aliyepigwa ni Amani Elisha (10) ambaye ni mwanafunzi wa Shule ya
Msingi Maarifa iliyoko Ukonga, Dar es Salaam, baada ya kipigo alizimia
siku mbili.
Tukio
hilo la kikatili lilitokea usiku wa Ijumaa iliyopita na sababu ya mtoto
huyo kupewa kipigo inadaiwa ni kutokana na utoro shuleni na kwamba hata
akienda huwa haandiki.Waandishi wetu waliponasa tukio walimtafuta mama
mzazi wa mwanafunzi huyo maarufu kama mama Amani na mahojiano yakawa
hivi:
ALIMPA KICHAPO KIKALI
Mwandishi: Mama ni kweli kuwa mume wako alimpiga mtoto wenu?
Mama Amani: Ni kweli baba yake Amani ndiye aliyempiga.
Mwandishi: Kwani huyu ni baba yake mzazi?
Mama Amani: Ni baba yake mzazi kweli, wakumzaa.
Mwandishi: Wakati mtoto anapigwa wewe ulikuwepo?
Mama
Amani: Hapana, sikuwepo nyumbani, nilikuwa kwenye shughuli zangu,
niliporudi nikakuta haya. Niliambiwa na majirani kuwa Amani kapigwa na
baba yake. Hakukuwa na jinsi, tulimpeleka mtoto hospitali kutibiwa baada
ya kuzimia.
Ilidaiwa
kuwa baba yake aliamua kumpa adhabu mwanaye baada ya kubaini kuwa
alikuwa hafiki shuleni na hata akifika alikuwa haandiki chochote na
alipofuatilia, walimu walimthibitishia.
“Ni kweli huyo baba aliwahi
kufika hapa shuleni akathibitishiwa kuwa mwanaye ni mtoro na hata
akifika ni mvivu kwani haandiki chochote.
“Alipoambiwa
hivyo alipatwa na hasira na kutaka kumchapa hapahapa shuleni lakini
hatukumruhusu. Tulimuambia kama ni kumchapa akafanye hivyo nyumbani
kwake,” alisema mwalimu mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina lake
gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa shule.
Mtoto Amani Elisha akiwa amelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
JIRANI ASIMULIA
Jirani
mmoja aliyeshuhudia kichapo hicho aliwaambia waandishi wetu kuwa Elisha
au baba Amani ni jirani yao lakini walishangazwa na kichapo alichokuwa
akimpa mtoto wake.
“Alimpiga kwa muda mrefu na hakuna hata jirani
aliyetoa msaada, kila mtu aliamua kukaa pembeni huku tukishangaa kipigo
alichompa mtoto huyo.
“Mtoto
huyo alipigwa hadi kuzimia lakini baadaye alizinduka na mama yake
aliporejea, kwa kushirikiana na majirani waliamua kumpeleka hospitali,”
alisema shuhuda huyo.
Jirani mwingine ambaye hakupenda jina lake
liandikwe gazetini aliyeongozana na mama huyo kwenda hospitali, alisema
kufuatia hali ya mtoto kuwa mbaya waliambiwa waende polisi wakachukue
PF3 ndipo angetibiwa.
WATINGA POLISI
Baada
ya kufika katika Kituo cha Polisi cha Stakishari, Ukonga na kutoa
taarifa ya tukio hilo waliandikiwa PF3 na kumpeleka Amani Hospitali ya
Amana kwa ajili ya matibabu lakini kufuatia hali yake kuwa mbaya
alihamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
AFANYIWA UPASUAJI WA KICHWA
Gazeti
hili lilimfuatilia mtoto huyo katika Hospitali ya Muhimbili na kukuta
amelazwa wodi A, katika Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi)
akiendelea na matibabu.
“Ni
kweli mtoto huyo anapatiwa matibabu na amefanyiwa upasuaji wa kichwa na
hali yake inaendelea vizuri,” alisema daktari mmoja ambaye hakutaka
jina lake kuandikwa gazetini.
BABA MBARONI
Baba wa Amani anashikiliwa katika Kituo cha Polisi Stakishari, Ukonga, Dar es Salaam huku uchunguzi wa tukio hilo ukiendelea.
Gazeti hili linampa pole mtoto Amani na tunamuombea apone haraka ili arejee shuleni kuendelea na masomo pamoja na wenzake.