TUKIO la
kutisha la kushambuliwa kwa Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe
mkoani Geita, ambapo askari wawili walipoteza maisha na silaha kadhaa
kuporwa, limeelezwa kuwa kwa kiwango cha asilimia mia moja, jambo hilo
ni ugaidi wa dhahiri.
Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Bukombe mkoani Geita, kilichoshambuliwa kwa mabomu.
Jumamosi
iliyopita, majira ya saa sita usiku, watu wasiojulikana, walikivamia
kituo hicho kwa mabomu na silaha zingine nzito zinazosadikika kuwa ni za
kivita, wakafanya mauaji na kujeruhi watu wengine kadhaa kabla ya
kupora bunduki na silaha zilizohifadhiwa kituoni hapo.
Damu ya maaskari iliyomwagika kwenye shambulia hilo la kigaidi.
“Huu
siyo ujambazi wa kawaida uliozoeleka, ni kweli kuna wakati matukio
yanatokea kuwa ya kutisha sana, lakini aina hii ya mashambulio siyo
kawaida, tena kituo cha polisi? Hawa watu ni dhahiri walihitaji kupata
silaha tu, sasa sijui zinakwenda kutumika wapi na tuna shaka kama hawa
si Watanzania,” alisema Zebareta Shayo, mkazi wa Sinza, jijini Dar es
Salaam.
Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, (IGP) Ernest Mangu (mwenye suti nyeupe) akiwa eneo la Tukio.
Waziri
Salum, mwanasheria na wakili wa kujitegemea alisema tukio hilo ni
vizuri kama lingeifanya serikali kutazama upya mipaka yetu kwani kuna
kila dalili kuna baadhi ya wageni wanaingia kirahisi na kufanya unyama
huo bila kujulikana.
Mfano wa silaha zilizoibwa na majambazi.
Askari
waliopoteza maisha katika shambulio hilo wametajwa kuwa ni Uria
Mwandiga mwenye namba WP 7106 na Dustan Kimati mwenye namba G 615 PC.
Majeruhi ni David Ngupama Mwalugelwa (44) namba E 5831 APL na Mohamed
Hassan Kilomo (25) namba H 627 PC.
Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) Isaya Mngulu.
Taarifa
kutoka eneo la tukio zinasema kuwa baada ya Mkuu wa Jeshi la Polisi
nchini, (IGP) Ernest Mangu na Mkurugenzi wa Mashtaka (DCI) Isaya Mngulu
kuwasili tangu juzi mkoani hapa, askari zaidi kutoka Mikoa ya Tabora,
Shinganya na Mwanza wanaendelea kuwasili.
Msako
mkali unaendeshwa na Jeshi la Polisi mkoani hapa kuweza kuwabaini
wahalifu hao huku Kamanda wa Mkoa wa Geita, Joseph Konyo akiwataka
wananchi kutoa taarifa mara moja watakapotilia shaka nyendo za mtu
yeyote ili kurahisisha zoezi hilo alilodai lazima lifanikiwe.
Juni
10, mwaka huu, tukio kama hilo likihusisha majambazi waliokisiwa kuwa
sita, wakiwa na pikipiki tatu walivamia Kituo Kidogo cha Polisi Mkamba
kilichopo Kimanzichana, Wilaya ya Mkuranga, Pwani na kuua askari mmoja
na mgambo na kujeruhi mgambo mwingine kisha kupora bunduki tano na
risasi 60.