
Shirika
la Viwango Tanzania (TBS) limesema kuwa litaendelea kuwabana
wafanyabiashara wanaoingiza nguo za mitumba za ndani zilizopigwa
marufuku ili kuhakikisha kwamba biashara hiyo inakoma nchini.
Hayo yalisemwa na Ofisa Uhusiano wa shirika hilo, Rhoida Andusamile jijini Dar es Salaam.
Andusamile
alisema wapo wafanyabiashara ambao sasa wanafanya ujanja wa kuchanganya
nguo za mitumba za kawaida na za ndani ili zisionekane kuwa zimo
zilizopigwa marufuku.
Alisema
kuwa katika ujanja huo, wafanyabiashara wanaoingiza marobota wamekuwa
wakizichanganya nguo kwa ufundi ili zionekane za aina moja huku wakiwa
wameweka nguo za ndani za kike na kiume zilizopigwa marufuku.
"Tunapobaini
hilo huwa tunaziteketeza na tunaendelea kufanya hivyo kadiri
inavyowezekana ingawa kwa sasa wapo baadhi ya wafanyabiashara wakubwa
wanaotumia njia za panya kuingiza bidhaa hizo nchini," alisema.
Alisema
kuwa sasa wanatumia njia za panya baada ya kubanwa bandarini na maeneo
mengine yakiwamo ya mipakani, hali ambayo kwa kiasi imepunguza wingi wa
uingizwaji wa nguo hizo.
Alisema
kuwa shirika hilo limekuwa likiwafuata wafanyabiashara hadi kwenye
maghala wanayohifadhia marobota ya nguo hizo na kufanya ukaguzi wa kina
na wanapobaini kuwapo kwa nguo zilizopigwa marufuku huziteketeza.
"Mwanzoni
wakati zoezi la kuondoa nguo hizo sokoni, walikuwapo wafanyabiashara
waliodai kuwa wana mzigo mkubwa wa nguo hizo wakaomba wapewe muda ili
waumalizie, lakini ajabu ni kwamba wanaendelea kuingiza nchini
kinyemela," alisema.
Alisema
kuwa TBS imeshagundua ujanja huo na ndiyo maana imekuwa ikiwafuatilia
kila kona ili kuhakikisha kwamba wanaacha kuingiza nguo hizo ambazo
kimsingi hazifai kuvaliwa.
Andusamile
alisema kuwa hatua ya kuondoa nguo hizo sokoni ni utekelezaji wa
matakwa ya agizo la Sheria ya 2009 inayozuia matumizi ya nguo za ndani
zilizokwisha kutumika.
Alisema
kuwa licha ya unafuu wa gharama za upatikanaji wa nguo hizo, shirika
hilo litaendelea kusimamia sheria na kupambana na wauzaji soksi, nguo za
kulalia, sidiria, chupi na nyingine nyingi za aina hiyo.
Hata
hivyo, alisema bado ipo haja ya kutoa elimu kwa jamii ili kuepuka nguo
hizo, kutokana na ukweli kwamba zimekuwa zikiwasaidia watu wengi hasa
wale wa kipato cha chini ingawa jambo la msingi ni afya.