MSANII
nyota wa muziki wa Bongo Flava nchini, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’
huenda akaingia matatani baada ya juzi kupanda jukwaani kutumbuiza
katika Tamasha la Serengeti Fiesta 2014 akiwa amevaa sare ya Jeshi la
Wananchi Tanzania (JWTZ), kinyume cha sheria.
Tangu
msanii huyo afanye hivyo, mjadala umeibuka kwa wengi wao kujiuliza nini
maana yake na kama alifanya hivyo kwa kibali maalumu au la, hasa
ikizingatiwa ni hivi karibuni Jeshi hilo lilitoa onyo kwa wasanii na
wengineo kutotumia mavazi hayo.
Mbali
ya Diamond, hata vijana wake nao walishambulia jukwaa wakiwa katika
mavazi hayo, akiwemo msanii aliyemshirikisha katika moja ya nyimbo zake,
Ney wa Mitego.
Wakati
shoo hiyo ikiendelea, baadhi ya mashabiki walianza kumzomea kila
alipoimba kabla ya video kubwa ambazo zilikuwa mbele ya jukwaa hilo
kuanza kuonyesha picha za mnato na video za mwanamuziki huyo akiwa
amevaa mavazi hayo huku akiwa kama askari ‘anayekoki’ risasi katika
katika bastora na baadaye katika bunduki ya kivita.
Kitendo
hicho, kilionekama kuwakera zaidi maelfu ya wapenzi na mashabiki wa
muziki waliokuwa wamejazana katika viwanja vya Leaders Club, huku kila
mmoja akiwa na tafsiri yake.
Baada
ya tukio hilo la juzi usiku, kitendo cha nyota huyo kuvalia mavazi hayo
ya JWTZ, kimeibua mjadala hadi katika mitandao ya kijamii kuanzia jana
asubuhi, ambapo picha za msanii huyo zikitumika kujenga hoja ya uhalali
wa kufanya hivyo, huku vijana kadhaa wanaokutwa nazo mitaani wakiteswa
vibaya na jeshi hilo.
Kwa
upande wake Diamond, alitoa taarifa ndefu katika ukurasa wake wa
Facebook na Instagram, akiishia kuelezea ni kwa nini alizomewa katika
shoo hiyo.
Tanzania
Daima ilipomtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius
Wambura juu ya kitendo cha msanii huyo, alisema alikuwa hajui chochote
na kuahidi kulifanyia kazi kama atapelekewa taarifa na wasaidizi wake.
Alipotafutwa
Kaimu Msemaji wa JWTZ, Meja Joseph Msanja, simu yake iliita bila
kupokelewa na alipotafutwa msaidizi wake, alikiri kupata taarifa na
kujionea kupitia shoo hiyo, huku akisisitiza bosi wake anaweza
kulizungumzia hilo.
Tukio
hilo limefanyika ikiwa ni siku chache tu tangu kijana mmoja aliyekuwa
amevalia mavazi ya kijeshi maeneo ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam,
kuvuliwa na kupewa adhabu ya kuogelea katika dimbwi la maji machafu
yaliyotuama.
Aidha,
msanii Gwamaka Kaihula ‘Crazy GK’ aliwahi kuhojiwa na Jeshi hilo kwa
kutumia mavazi ya kijeshi katika kibao chake cha Simba wa Afrika, ambapo
alijitetea pamoja na kuomba msamaha kwa kilichofanyika.
Kutokana
na wimbi la watu mbalimbali hasa wasanii kuvalia mavazi yanayofanana na
sare za jeshi hilo, hivi karibuni Kurugenzi ya Habari na Uhusiano Makao
Makuu ya JWTZ, ilionya kama ifuatavyo:
Kumejitokeza
kama fasheni kwa baadhi ya wasanii, hasa wanamuziki wa Bongo fleva,
kurekodi video zao wakiwa wamevaa sare za jeshi kama vile suruali,
viatu, fulana, kaptula, mabegi au kofia.
Inawezekana
kwa namna moja ama nyingine, baadhi ya watumiaji wa sare hizo
hawafahamu ni kinyume cha sheria ya nchi kukutwa nazo, ingawa kutokujua
sheria bado sio utetezi mbele ya mahakama.
Mtu
yeyote yule asiye na ruhusa ya kushona, kuuza au kuingiza nchini sare
za jeshi, atakuwa ametenda kosa, kwa hiyo atafikishwa mahakamani na
kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zilizopo.
Katika
uvaaji au uingizaji nguo, kama itatokea kwamba nguo hizo zinafanana kwa
aina yoyote ile na zile za Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania,
ikadhaniwa kuwa ni hizo, mtu huyo ana hatia na anastahili kufikishwa
mahakamani na kuhukumiwa kwa mujibu wa sheria zinazohusu sare za majeshi
zilizopo
ilifafanua taarifa hiyo.