UTAFITI
uliofanywa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA),
umeonyesha asilimia 55.5 ya wanaume katika Wilaya ya Kinondoni, Dar es
Salaam ni vinara wa ulevi wa pombe.
Akizungumza
na waandishi wa habari Dar es Salaam jana wakati wa uzinduzi wa ripoti
ya utafiti huo, Msimamizi wa Utafiti, Dk. Severine Kessy, alisema
kukithiri huko kwa ulevi kumesababisha ongezeko kubwa la vitendo vya
ukatili wa kijinsia.
Alisema hali hiyo inatokea kwa kuwa kuna uhusiano mkubwa kati ya pombe na vitendo hivyo.
Dk. Kessy alisema katika utafiti huo, wamebaini asilimia 45.4 ya wanaume wengine hawatumii kabisa.
Kwa upande wa kinamama, alisema ulevi umefikia asilimia 40, wakati asilimia 60 hawatumii pombe.
Alisema
katika utafiti huo, imebainika asilimia 44 ya watu wenye umri wa miaka
18-24, bila kujali jinsia ndio wanaokunywa zaidi pombe kuliko umri
wowote.
Dk.
Kessy alisema utafiti huo uliofanyika katika Wilaya ya Kinondoni pekee,
ulijikita zaidi maeneo makuu mawili; athari za pombe, upatikanaji na
uelewa kuhusu ulevi huo.
“Asilimia 48 ya watu waliohojiwa imeonyesha wana uelewa kuhusu pombe, wakati asilimia 51 hawajawahi kutumia.
“Kwa
upande mwingine, katika utafiti wetu tulibaini ongezeko la wasomi
linawiana na ongezeko la unywaji pombe ambapo wanafunzi na wale
waliohitimu kidato cha nne, cha sita na vyuo wanakunywa zaidi kulingana
na hatua za kimasomo.
“Tuliangalia namna watu wanavyoanza kutumia pombe na vishawishi, tukabaini mengi.
“Kwa
msingi huu, asilimia 39 walisema walianza wenyewe, asilimia 13
walijifunza kutoka kwa wazazi wao, asilimia 38 walifundishwa na marafiki
wa kawaida na asilimia 9 walishawishiwa na wapenzi wao,” alisema Dk.
Kessy.
Pamoja na mambo mengine, alisema asilimia 19 hadi 12 waliohojiwa ni watumiaji wa pombe kila siku.
Alisema
asilimia 19 inaonyesha wanakunywa mara mbili hadi nne kwa wiki na kila
wanapokwenda kunakouzwa pombe wanakunywa chupa mbili hadi nne.
Dk. Kessy alisema asilimia 63 ya walihojiwa walisema nyumba zao ziko chini ya hatua 100 kutoka sehemu ambazo pombe zinauzwa.
Alisema
utafiti huo pia ulibaini athari za unywaji pombe ambapo asilimia 30.8
waliwahi kunyanyaswa na watu waliokunywa pombe, asilimia tisa waliwahi
kufanya ngono baada ya kunywa pombe na asilimia tano walipewa talaka
kutokana na pombe.
“Kundi
la watoto ambao waliwahi kupigwa na mzazi au mlezi aliyekunywa pombe ni
asilimia 23, asilimia 26 ya walio kwenye ndoa waliwahi kupigwa na
watalaka wakati asilimia 44 waliwahi kupigwa wakiwa kwenye ndoa,”
alisema Dk. Kessy.
Alisema kwa upande wa afya, watumiaji wengi wameathirika kiafya.
Ofisa
Ustawi wa Jamii wa chama hicho, Gladness Munuo alisema wamekuwa wakitoa
fedha kusaidia watoto waliotelekezwa na wazazi wao.
Alisema
kuanzia Aprili hadi Agosti, mwaka huu asilimia 60 ya watu walioripoti
kesi zao kwenye chama hicho zimetokana na ulevi pombe.