TAFRANI
ilizuka usiku wa kuamkia jana katika Hospitali ya Mwananyamala,
Kinondoni jijini Dar es Salaam, ikihusisha wanandoa baada ya mke
aliyekuwa amempeleka mtoto kutibiwa, kumbamba mumewe akimleta anayedaiwa
kuwa kimada pia kupata matibabu hospitalini hapo.
Mwandishi
ambaye alikuwa hospitalini hapo saa 5 usiku, alishuhudia mke huyo
anayedaiwa kuwa wa ndoa akimpiga ngumi ‘nyumba ndogo’ kabla ya kumvamia
mumewe na pia kumpiga ngumi akitaka amweleze mwanamke aliye naye ni
nani.
Mwanamke
huyo ambaye jina lake halikupatikana, alikuwa na mtoto anayekadiriwa
kuwa na umri wa miaka mitatu ambaye alidai alizidiwa usiku bila mumewe
kuwepo.
Akisimulia
watu waliokusanyika kushuhudia tukio hilo, mwanamke huyo
aliyejitambulisha kuwa mkazi wa Mwananyamala, alidai baada ya mwanawe
kuzidiwa, alimpigia mumewe ambaye hakupokea simu, akitaka kumfahamisha
ugonjwa arudi nyumbani wasaidiane kumpeleka hospitali.
“Nilipoona simu imezimwa kabisa,
nikaamua kuchukua pikipiki haraka nikampeleka mtoto zahanati na
wakaniambia nimlete hapa (Mwananyamala),” alisema.
Aliendelea kusimulia, “nimefika
nimefungua jalada, nimekaa kusubiri kumwona daktari, nashangaa namwona
mwanaume anaingia huku amemkumbatia mwanamke aliyekuwa hawezi kutembea
akigugumia kama mgonjwa mahututi,” alieleza mama huyo anayekadiriwa kuwa
na umri wa miaka 28.
Baada ya kumwona mumewe akiwa na
mwanamke huyo amemwegemea kifuani, nao wakisubiri utaratibu wa kumwona
daktari, mke huyo halali alinyanyuka taratibu na kuomba ashikiwe mtoto.
Huku akimkaba mumewe, mwanamke huyo
alisikika akisema, “Nataka uniambie huyu ni nani, yaani mimi nateseka na
mtoto nyumbani, anaumwa, nakutafuta usiku huu sikupati, ukanizimia na
simu, kumbe uko kwa malaya wako, niambie ni nani huyu la sivyo
utanitambua.”
Watu waliokuwepo waliingilia kati na kumshika huyo mwanamke wa ndoa wakimtaka apunguze hasira.
Wakati akimng’ang’ania mumewe huku
akitaka ufafanuzi, mwanamke aliyedaiwa kuwa kimada, ambaye awali alifika
hospitalini hapo akiwa ameshikiliwa kwa kutojiweza kutokana na ugonjwa,
alitumia nafasi hiyo kutimua mbio na kuondoka katika eneo la hospitali
asijulikane alikoelekea.
Baadhi ya madaktari na wauguzi waliokuwa
zamu na watu waliokuwepo hospitalini hapo, waliwaongoza wanandoa hao
kutoka nje kwa kile kilichosadikiwa ni kwenda kuzungumza na kumaliza
tofauti zao.