Audrey Mbugua akiwa nje ya mahakama ya awali.
MAHAKAMA
Kuu imeamuru Baraza la Kitaifa la Mitihani Kenya (KNEC), libadilishe
jina cheti cha mlalamikaji ambaye amekuwa akipigana atambuliwe kuwa
mwanamke.
Jaji
Weldon Korir jana Jumanne aliagiza KNEC impe cheti kipya Bi Audrey
Mbugua kikiwa na jina jipya lililochapishwa katika gazeti rasmi la
serikali.
Mlalamikaji, ambaye awali alitambuliwa kwa jina Andrew Ithubu Mbugua, alibadilisha jina lake kuwa Audrey Mbugua.
Bi
Mbugua aliishtaki KNEC kwa kukataa kubadilisha jina lake na kuondoa
neno “mwanaume” katika cheti chake kuonyesha kuwa ni “mwanamke” hata
baada ya kuonyesha gazeti rasmi la serikali lililochapisha mabadiliko
kwenye jina lake.
Jaji Korir ameipa KNEC siku 45 kutayarisha cheti kipya na kumpa Bi Mbugua kikiwa na jina lake jipya.
Jaji
aliamuru herufi “M” ambayo inamaanisha “mwanaume” iondolewe katika
cheti nambari 1855399 ambacho Bi Mbugua alipewa na KNEC kwa jina la
Ithubu Andrew Mbugua.
Jaji
aliamuru cheti hicho kitolewe upya kwa jina jipya la “Audrey Mbugua”
bila herufi “M” (mwanaume) ama “F” (mwanamke) akisema herufi hizo
haziongezi maana au thamani yoyote kwa cheti hata zikitolewa.
“Mlalamikaji
ni mwanamke ambaye amegubikwa kwenye mwili wa mwanamume ... maumbile ya
kike ndani yake yanazidi yale ya kiume na sina budi kuamuru mlalamikaji
ajihisi mkamilifu,” alisema Jaji Korir.
Jaji
alisema katiba inaelezea wazi kwamba “kila mtu anatakiwa kuchukuliwa
kwa heshima na lazima kipengee hiki kimfaidi mlalamishi kabisa.
Kutokitekeleza kwa manufaa yake ni kukiuka haki zake.”
Alisema
kama Audrey atajihisi “mzima” ni lazima akubalike jinsi alivyo na
kumnyima haki ya kubadilisha jina lake ni kukiuka haki zake na uhuru
aliopewa na katiba.
Wakili
wa Audrey, Bw Colbert Ojiambo, aliIambia mahakama kuwa mlalamikaji
alizaliwa jinsia yake ikiwa na utata na amekuwa akitibiwa katika
hospitali moja Nairobi.
Jaji Korir alisema ameangalia kesi nyingine za aina hiyo na kufikia uamuzi kwamba zote zinaegemea haki na heshima kwa binadamu.
“Mlalamikaji
aliwasilisha mahakamani gazeti rasmi la serikali lililochapishwa
Januari 19, 2012 ambapo jina lake limebadilishwa kuwa Audrey na Mkuu wa
Sheria akasema hapingi kubadilishwa kwa jina lake,” akasema jaji.
Alisema
sheria nambari 9(1) ya mitihani inasema cheti kinachotolewa na KNEC
kinafaa kuonyesha jina la mwanafunzi, nambari ya usajili na masomo
aliyofanya, alama alizopata na kwamba kinatolewa kwa utaratibu fulani.
Jaji
Korir alisema sheria inaruhusu mabadiliko kufanyiwa cheti na kwamba
herufi ya kuonyesha jinsia haina maana wala si lazima iwepo.