Ili
uweze kuwa na furaha maishani, lazima uwe katika uhusiano imara
usiotetereka. Kama unaishi na mke au mume ambaye moyo wako umemchagua
lazima furaha itatawala katika nyumba yenu. Lakini rafiki zangu, huwezi
kuwa katika ndoa yenye furaha kama hukuwa na mchumba bora. Kwa maneno
mengine, lazima uanze kuboresha uchumba wako kwanza, uwe na uhakika
kwamba mwenzi uliyenaye ni sahihi ili ukiingia kwenye ndoa usijute.
Mapenzi ni sawa na bustani nzuri ya maua rafiki zangu, wakati mwingine inahitaji mbolea, kumwagiliwa maji na hata kupaliliwa.
Kwa
kufanya hivyo utazidisha ladha ya mapenzi na kuyafanya yazidi kuwa na
nguvu zaidi ya awali. Lakini kama hutamwagilia, hutaweka mbolea,
hutapalilia, hesabu kwamba mapenzi yako yanaweza kuanza kupoteza nguvu
taratibu na hatimaye kufa kabisa.
Kikubwa
ambacho nimepanga kuzungumza nanyi leo ni jinsi ya kumpagawisha mwenzi
wako ili awe wako peke yako. Umeshawahi kufikiria kwamba, kama
ukishindwa kutimiza mambo fulani katika penzi au ndoa yako, mwenzi wako
anaweza kuwa wa kushea?
Kama
bado, inakubidi ufahamu hilo kuanzia leo. Mpenzi anahitaji mambo mengi
ili aendelee kuwa mwaminifu kwenye penzi lenu. Ni kweli kwamba uaminifu
upo kwa mtu mwenyewe, kama mtu ni mwaminifu basi atadumisha uaminifu
uliopo ndani yake, lakini kama kuna mambo unakosea, lazima utasalitiwa!
Tena
basi, kama mwenzi wako anakupenda, atakusaliti huku analia! Kwanini?
Kwasababu analizwa ba kitendo ambacho hajapenda kukifanya ila wewe
mwenyewe ndiyo umemlazimisha afanye hivyo.
Kuna nini zaidi katika dhana ya usaliti?
Tukiachana
na tamaa, hulka na ushawishi, wakati mwingine mpenzi anaweza kusaliti
kwa kukosa yale ya muhimu zaidi katika penzi au ndoa yake.
Kwa
bahati mbaya sana, watu wa aina hii huwa hawasemi moja kwa moja kuwa
wanakosa vitu fulani au wanapenda vitu fulani, badala yake hutumia lugha
za ishara zaidi na kama hutaelewa basi huona suluhisho ni kutafuta
pumziko lingine.
Hapa
sasa mwenzi wako anakuwa si wako peke yako tena! Lakini lazima
uhakikishe mpenzi wako anaendelea kuwa wako bila kushea na mtu yeyote na
jambo hili linawezekana kabisa ikiwa wewe mwenyewe utataka iwe hivyo.
Zipo
hatua au mambo mengi ya kumfanyia mpenzi wako ili awe wako peke yako,
lakini hapa nitakupa yale ya msingi zaidi yatakayokusaidia katika penzi
lako.
Njia
hizi za siri nimezifananisha na shamba au bustani, ambayo ina mahitaji
yake. Sasa katika uchambuzi huu, nitaainisha jinsi ya kuitunza bustani
hii ya mapenzi ili kuifanya bora zaidi kila siku.
Kitu
cha kwanza kabisa ni mbelea. Hapa nazungumzia penzi ambalo tayari
limeshakuwa penzi! Kama ni bustani basi tayari mboga zako zimemea
vizuri.
Lakini ukumbuke kwamba, bustani yako haitaweza kuendelea kuwa bora kama haitakuwa na matunzo. Hapa penzi linahitaji mbolea.
Mbolea
ninayoizungumzia hapa ni maneno matamu yaliyojaa huba. Fikisha hisia
zako kwa mwenzi wako kwa namna ya kipekee iliyojaa penzi la dhati.
Mweleze
jinsi unavyompenda na jinsi maisha yako ambavyo hayawezi kukamilika
bila yeye. Huu ni wakati wako wa kumsumbua kwa meseji zilizojaa tungo za
mahaba, kadi, maua na zawadi ndogo ndogo.
Baadhi
ya wanandoa wakishaoana, huacha utaratibu huu. Kuna wanaosema: “Ah!
Hayo mambo ya kizamani bwana, kipindi akiwa demu wangu, sasa hivi yupo
ndani, kwanini nihangaike?”
Haya ni makosa makubwa ndugu yangu. Shamba bila mbolea kuna mavuno kweli? Huwezi kuvuna.
Kitu
kingine muhimu katika bustani, kama ujuavyo mpenzi msomaji wangu ni
maji. Bustani yako itahitaji maji kwa ajili ya kuzidisha ustawi wa mazao
yako. Hapa unatakiwa kuwa mbunifu zaidi katika mambo yanayohusu mapenzi
moja kwa moja.
Unatakiwa
kubadilisha aina ya ufanywaji wa mapenzi, mahali pa kukutana na hata
sehemu za mitoko. Inashauriwa ili kuboresha penzi ni vizuri kutoka
sehemu mbalimbali na mwenzi wako. Inapendeza zaidi angalau mara tatu kwa
miezi sita, kulala na mwenzako hotelini.
Hapa utakuwa unanakshi zaidi penzi lako. Outing yako ni vyema ikawa ya kimahaba zaidi, kuanzia mavazi, sehemu mnazotembelea n.k
Mfanyie mwenzi wako mambo ya kimahaba sana mnapokuwa wawili. Mbusu,
mkumbatie, mwambie jinsi unavyojisikia wa pekee kuwa wake. Utundu wako
wote umalizie hapa, ukifanya hivyo utakuwa umemwagilia bustani yako
vyema.
Baada
ya muda bustani huota majani mengine ambayo si mboga! Yawezekana
kabisa, kwa bahati mbaya uchafu ukaingia bustanini. Wakati wa palizi ni
muda sahihi wa kuondoa vyote hivyo.
Hata katika mapenzi pia hutakiwa kufanya jambo hili. Kugombana au kupishana kiswahili kwa wapenzi ni jambo la kawaida sana, hivyo ni vyema kuweka sawa tofauti hizo mapema, kabla tatizo halijawa kubwa zaidi. Hii ndiyo palizi ninayoizungumzia.
Usikae na kinyongo moyoni mwako, kuwa
mjanja, hata kama ni yeye ndiye aliyekosea, zungumza naye ukimweleza
jinsi ambavyo hupendi mgombane, mkimweleza hisia zako kwamba unatamani
sana muelewane katika siku zote za maisha yenu. Weka mambo sawa.
Kwa
kufanya hivi, kwa hakika penzi lako litazidi kuwa imara zaidi na
atakuwa wako peke yako. Mapenzi ni utundu kidogo tu rafiki zangu.