SIKU chache
baada ya kutolewa kwa taarifa ya kukamatwa kwa promota aliyempeleka
msanii Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ nchini Ujerumani kwa ajili ya
kufanya shoo aliyejulikana kwa jina la Awin Williams Akpomiemie, mwenye
asili ya Kinigeria, nyuma ya sakata hili siri saba zimefichuka, Risasi
Jumamosi lina ripoti kamili.
Mashabiki wenye gadhabu wakilizingira gari la Mbongo Fleva, 'Diamond Platinum' nchini Ujerumani.
SIRI YA KWANZA; KIBALI
Uchunguzi
uliofanywa na mwanahabari wetu ulibaini kwamba katika sakata hilo
lililojiri wiki mbili zilizopita, promota huyo aliwadanganya wamiliki wa
Ukumbi wa Sindelfingen uliopo Mji wa Stuttgart, Ujerumani kuwa kutakuwa
na mkutano wa Waafrika waishio nchini humo na baada ya hapo kutakuwa na
pati ya kawaida.
Ilisemekana
kwamba wamiliki hao walitoa kibali kwa ajili ya mkutano hivyo
walishtushwa kuona ukumbi umejaa na watu wanamsubiri Diamond kinyume na
makubaliano.Kikizungumza kwa njia ya simu kutoka nchini humo, chanzo
chetu kilidai kwamba ujanja alioutumia Awin kuwadanganya wamiliki wa
ukumbi huo ndiyo chanzo cha fujo hiyo kwani alishindwa kuanza shoo
mapema kwa kuwa wamiliki wa ukumbi hawakuwa tayari kwa jambo hilo.
Magari ya wagonjwa yakiwa tayari kuhudumia majeruhi eneo la tukio.
“Unajua
siyo kila mtu anataka kuishi kwa shaka huku Ujerumani. Kila mtu anajua
maisha ya Waafrika jinsi wanavyoishi, sasa uongo ungebainika mapema
sidhani kama tungeishi kwa raha,” kilidai chanzo hicho.
SIRI YA PILI; UTEKAJI
Habari
kutoka nchini humo zilidai kwamba siri ya pili ni kwamba Diamond
alikuwa atekwe kwani kulikuwa na waandaaji watatu wa mpango huo hivyo
wawili walitaka kumteka msanii huyo ili akafanye shoo sehemu nyingine.
“Mbali
na Awin kulikuwa na jamaa wengine wawili ambao waliingilia mchakato
mwishoni wakitaka waandae shoo hiyo lakini mwishoni walitofautiana ‘so’
walitaka waharibu ndiyo maana Diamond akachelewa ukumbini na vurugu
zikatokea,” kilitonya chanzo chetu.
Mkali 'Diamond' akisepa kutoka eneo la tukio.
SIRI YA TATU; BIMA
Kikiendelea
kutiririka, chanzo hicho kilidai kwamba ukiachana na uongo wa promota
Awin iligundulika kwamba hakukuwa na bima ya kulinda usalama wa watu
hasa endapo lingetokea tatizo kama lililotokea ambapo wengi
walijeruhiwa.
“Huku
Ujerumani huwezi kufanya onesho lolote bila bima ya kulinda usalama
kwenye shoo yako, sasa jamaa hakuwa nayo, kosa ambalo ni kubwa sana kwa
sheria za Ujerumani,” alisema mtoa habari wetu.
SIRI YA NNE; UKUMBI WA MIKUTANO
Kingine
kilichogundulika ni kwamba hata ukumbi wenyewe ulikuwa wa mikutano na
maonesho ya bidhaa na si wa kufanyia shoo za muziki kama alivyotaka
kufanya yeye.
“Ukumbi
wa Sindelfingen, Stuttgart ni wa mikutano na maonyesho ya bidhaa,
haujawahi kutumika kwa shoo kama ile ndiyo maana hata sisi tulishangaa
iweje utumike kwa ajili ya shoo ya Diamond?” kilihoji chanzo chetu.
Moja ya shoo aliyofanikiwa kufanya('Diamond') huko majuu.
SIRI YA TANO; HASARA MIL. 600
Chanzo
hicho kilieleza kwamba baada ya uchunguzi wa polisi, ilibainika kwamba
hasara iliyosababishwa na vurugu hizo inafikia euro 300,000 (zaidi ya
Sh. milioni 600 za Kibongo).
“Hicho ndicho kiasi ambacho Awin
anatakiwa kukilipa kwa wamiliki wa ukumbi kwani alisababisha loss
(hasara) kubwa sana,” kilidai chanzo hicho.
SIRI YA SITA; KESI
Licha
ya promota huyo kufikishwa polisi kwenye Mji wa Stuttgart, suala lake
lipo chini ya ofisi ya mji huyo ili sheria ichukue mkondo wake huku
polisi wakisisitiza kwamba Diamond akitia mguu tu watamdaka.
“Hadi
ninavyoongea na wewe polisi bado wanamuhoji Awin kutokana na tetesi
kwamba anajihusisha na biashara tata lakini kuhusu fujo zile kesi yake
iko chini ya ofisi ya Mji wa Stuttgart, inavyooneka hali iko vibaya sana
kwa upande wake na Diamond kwani polisi wanakomaa kuwa akitimba tena
watamkamata,” kilisema chanzo hicho.
'Diamond' akiwa na Meneja wake, Babu Tale.
SIRI YA SABA; KUTAFUTA ‘KIKI’
Uchunguzi
mwingine wa gazeti hili ulibaini kwamba sakata la vurugu za Diamond
nchini Ujerumani lilipangwa kwa makusudi ili kutafuta ‘kiki’ (umaarufu)
na kuvuta hisia kupitia vyombo vya habari vya kimataifa ili kumpaisha
zaidi.
“Fuatilia
majibu ya meneja wake, Babu Tale. Alisema kuwa vurugu zilikuwa mbaya
lakini ni fagio kwa Diamond kimataifa. Kama siyo kutafuta kiki ni nini?”
kilihoji chanzo makini Bongo na kuongeza:
“Nasikia anarudi Ujerumani kufanya shoo kubwa ya bure (Septemba 20). Wewe huoni hapo kulikuwa na mchezo?”
DIAMOND ANASEMAJE?
Alipoulizwa
Diamond kuhusiana na utayari wa yeye kurudi Ujerumani na yote
yaliyotokea, hakutaka kufungukia zaidi ishu hiyo na kudai amejiaandaa
vilivyo kufanya shoo ya bure Septemba 20 kama waandaaji walivyomtaka.
TUMEFIKAJE HAPA
Agosti
30, mwaka huu zilitokea fujo kwenye Ukumbi wa Sindelfingen uliopo Mji
wa Stuttgart, Ujerumani zilizosababishwa na Diamond ambaye alichelewa
kupanda stejini hadi saa 10:00 alfajiri ambapo watu walivunja viti,
vyombo vya muziki na vitu mbalimbali baada ya mashabiki kushikwa na
hasira kwa kukosa burudani ya shoo Diamond.