Ajali
mbaya iliyosababisha vifo vya watu 39 iliyohusisha Basi la Kampuni ya
J4 Express lenye nambari za usajili T 677 CYC, lililokuwa likitoka
Musoma kuelekea Sirari mkoani Mara baada ya kugongana uso kwa uso na
basi lingine la Kampuni ya Mwanza Coach lenye nambari za usajili T 736
AWJ katika eneo la Saba Saba mjini Musoma mkoani Mara, Ijumaa iliyopita,
imedaiwa kuna ushirikina au kafara ndani yake.
Umati wa watu uliofurika kushuhudia ajali mbaya ya basi iliyotokea Musoma.
Baadhi
ya mashuhuda wa ajali hiyo waliliambia Ijumaa Wikienda kwamba kuna
kafara ilitolewa na mmoja wa watu waliohusika katika ajali
hiyo.“Haiwezekani magari yakagongana uso kwa uso sehemu nyeupe kama ile,
hata kama ni uzembe, ajali hii ni zaidi ya uzembe,” alisema kijana
mmoja aliyeshuhudia ajali hiyo aliyeomba hifadhi ya jina lake kwa imani
hiyo ya kishirikina.
Aliongeza kwamba kuna wafanyabiashara wengi walikuwa kwenye mabasi hayo na baadhi yao wanapenda mambo ya kishirikina.
Baadhi ya miili ya watu waliofariki katika ajali hiyo.
Hata hivyo, alipobanwa zaidi, hakuwa tayari kutoa ufafanuzi.
Shuhuda
mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la Maduhu alidai kuwa chanzo
cha ajali hiyo ni basi la J4 ambalo lilikuwa likijaribu kulipita gari
dogo aina ya Nissan Terano lenye nambari za usajili T 332 AKK katika
sehemu ambayo mbele kulikuwa na daraja linaloweza kupitisha gari moja
kwa wakati mmoja.
Guldoza
likifanya kazi ya kuichomoa gari ndogo aina ya Nissan Terano lenye
namba ya usajili T 332 AKK lililosukumwa na basi kwenye ajali hiyo mpaka
kuingia mtoni. Gari hili ilikuwa na watu watatu, ambapo wawili
wamefariki dunia na mmoja kujeruhiwa.
“Ukweli
wapo watu wanadai kuwa hii ni kafara ili majini wanywe damu na mambo
yao yaende vizuri lakini ukweli ni kwamba basi hilo lilikuwa kwenye
mwendo kasi, lililisukuma ubavuni gari dogo ambalo halikuweza kuhimili
na kutoka kwenye njia na kwenda kuingia mtoni nalo kugongana na basi la
Mwanza,” alisema Maduhu.
Jumamosi
iliyopita, gazeti hili lilipokea ripoti kuwa bado haijafahamika ndani
ya mabasi hayo kulikuwa na abiria wangapi ambapo ilidaiwa kuwa waliokufa
na majeruhi walikuwa wameongezeka.