MTOTO Happiness
Kashinje (9) (pichani)aliyekuwa mwanafunzi wa darasa la tatu katika
Shule ya Msingi Negezi mjini Shinyanga, ameokotwa akiwa amekufa baada ya
kudaiwa kutekwa na watu wasiojulikana kabla ya kubakwa na kutobolewa
macho.
Mtoto Happiness Kashinje (9) pichani kulia enzi za uhai wake.
Tukio hilo lilijiri hivi karibuni Nhelegani, Kata ya Kizumbi kilometa chache kutoka nyumbani kwao.
Habari
zilizofika Uwazi kuhusu mkasa huo zinasema, Happiness aliyekuwa akiishi
na shangazi yake, alipotea Agosti 27, mwaka huu baada ya kuaga kuwa
anakwenda saluni kupunguza nywele na hakurudi tena hadi siku iliyofuata
mwili wake ulipookotwa ukiwa umeanza kuharibika.
Tukio
hilo la kinyama lilmegusa hisia za wakazi wengi wa Manispaa ya
Shinyanga hasa ikizingatiwa kuwa mwishoni mwa mwaka jana, muuza urembo
mmoja alikamatwa kwa tuhuma za kuwabaka na kuwatoboa macho wanafunzi
wanne wa shule za msingi za Manispaa ya Shinyanga. Mtuhumiwa huyo
alihukumiwa kifungo cha maisha jela.
Baadhi
ya watoto walioathirika katika matukio ya ubakaji uliofanyika katika
maeneo tofauti ya Mji wa Shinyanga walilazwa kwa muda mrefu katika
hospitali ya mkoa na wengine kupelekwa Bugando jijini Mwanza lakini hata
hivyo, baadhi yao macho yao yameathirika.
Kwa
mujibu wa maelezo ya mlezi wa mtoto Happiness, John Njai ambaye ni mume
wa shangazi yake, siku moja kabla ya tukio, marehemu aliomba shilingi
mia tano kwa ajili ya kunyolea nywele.
Baada
ya kupewa hela hiyo inadaiwa bibi yake alimtaka anyoe nywele hizo
nyumbani ili fedha hiyo itumike kwa matumizi mengine, lakini alikataa
kwa madai kuwa angenyolewa vibaya na hivyo kuchekwa na wenzake shuleni.
Bibi
huyo alimruhusu mjukuu wake kwenda saluni na kwamba akiwa njiani
anarudi aliomba lifti kwa watu wawili waliokuwa kwenye baiskeli moja
lakini walimnyima kwa madai ya kukosa kiti cha nyuma.
Baada
ya kuchelewa kurudi nyumbani, wazazi na walezi walipata wasiwasi hivyo
kuanza kumfuatilia kwa ndugu na majirani, lakini hawakufanikiwa licha ya
kutoa tangazo msikitini juu ya kupotea kwa binti huyo.
Pia
walitoa taarifa kwa mwenyekiti wa mtaa, Kituo cha Polisi cha Nkomo na
kwa ndugu na jamaa wanaowafahamu na hatimaye Agosti 28, mwaka huu, mtu
mmoja alisema mwili wa mtoto wa kike anayekadiriwa kuwa na miaka tisa au
kumi umeokotwa katika Kijiji cha Nhelegani ukiwa umeharibika.
Polisi
waliuchukua mwili huo kwa ajili ya uchunguzi, baadaye waliruhusu
mazishi yake huku hofu na simanzi zikiwa dhahiri kwenye nyuso za ndugu,
jamaa na marafiki. Hapiness alizikwa katika makaburi ya familia yaliyoko
kijijini Negezi.