LICHA
ya kusababisha vifo vingi duniani ikiwemo Tanzania, shinikizo la damu
(High Blood Pressure), inaelezwa na wataalamu kuwa ndiyo chanzo cha
magonjwa mengine hatari ya moyo, kiharusi na figo. Hata hivyo ugonjwa
huu unaweza kuzuilika na kutibika kwa njia asilia, mbali na matibabu ya
kawaida.
POTASIAMU MWILINI
Ulaji
wa mboga na matunda yenye kiwango kingi cha Potasiamu (Potassium) ni
sehemu muhimu sana katika mikakati na mipango anayoweza kuwa nayo mtu ya
kudhibiti au kushusha kiwango cha shinikizo la damu alichonacho, hii ni
kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Profesa wa Tiba za Kinga, Dk. Linda
Van Horn wa Chuo Cha Tiba cha Feiberb.
Profesa
huyo anasema kuwa ulaji wa Potasiamu kati ya miligramu 2000 na 4000
kwa siku kutasaidia kushusha kiwango cha shinikizo la damu kwa kiasi
kikubwa. Vyakula vinavyoaminika kuwa na kiwango kingi cha Potasiamu ni
viazi vitamu, maharagwe, nyanya, juisi ya machungwa pamoja na karanga na
korosho.
KUWA MAKINI NA CHUMVI
Baadhi
ya makundi ya watu yanayougua ugonjwa wa shinikizo la damu, ulaji wa
chumvi kiasi chochote huwa na athari mbaya kwao, hasa wale wenye
historia ya kifamilia ya kuugua ugonjwa huu.
Kwa
kuwa siyo rahisi mtu mwenye shinikizo la damu kujitambua kama chumvi
ina muathiri zaidi, inashauriwa kila mtu kupunguza matumizi ya chumvi
katika vyakula vya kila siku.
Kwa
mujibu wa mtaalamu wa masuala ya lishe ya moyo na mapafu, Dk. Eva
anasema kuwa kiwango cha chumvi cha wastani anachotakiwa kutumia mtu kwa
siku kisizidi miligramu 1,500. Kipimo hicho ni zaidi kidogo ya kijiko
kimoja cha chai ambacho huwa na miligramu 1200. Kwa maana nyingine,
matumizi ya mtu kwa siku nzima katika milo yote hayatakiwi kuzidi kijiko
kimoja na nusu cha chai.
ULAJI WA CHOKOLETI
Aina
nyingi za chokoleti (Chocolate) zina aina ya kirutubisho (flavanols)
kinacholainisha mishipa ya damu na kuwezesha damu kutembea vizuri
mwilini. Katika utafiti mmoja, asilimia 18 ya wagonjwa wa presha
waliokula chokoleti walionesha kupata ahueni kwa presha kushuka. Kiasi
cha chokoleti moja kinatosha kwa siku, muhimu iwe inayotengenezwa
kutokana na Cocoa.
TATIZO LA KUKOROMA USIKU
Kwa
mujibu wa utafiti wa Chuo Kikuu cha Alabama nchini Marekani, watu wengi
wenye tatizo la kukoroma usiku, wana homoni ijulikanyo kama
‘aldosterone’ ambayo huongeza shinikizo la damu na inakadiriwa kuwa nusu
ya watu wote wenye tatizo la kukoroma wana presha.
Mbali
ya kukoroma kama dalili moja wapo ya kuwa na presha kwa baadhi ya watu,
kusikia uchovu sana na kizunguzungu asubuhi nako ni dalili moja wapo,
hivyo inashauriwa kumuona daktari akushauri kuondoa tatizo la kukoroma
ili kujiepusha na matatizo yatokanayo na shinikizo la damu.
Kama hujui hali yako kuhusu presha, ni vyema ukamuone daktari na kupima sasa.