Wanafunzi leo naendelea na somo nililoanza wiki iliyopita.
Ifahamike
kwamba; ili uweze kuelewa somo lazima uzingatie mwalimu anapokufundisha
na uchukue hatua za kufuatilia dokezo zote zinazotolewa na ikiwezekana
muulize mwalimu wako mahali ambapo hujaelewa sawasawa. Achana na vitendo
vya kukwepa kufundishwa!
TATU: PUNGUZA WINGI WA MAELEZO
Wakati
mwingine ni kawaida kwa mwalimu kufundisha kwa kutumia mazungumzo
marefu yanayoambatana na notisi nyingi za kuandika; katika hali hiyo
mwanafunzi asitegemee kuelewa mambo yote hayo kwa wakati mmoja.
Mwanafunzi
wangu; jambo unalotakiwa kufanya katika mazingira ya namna hiyo ni
kuchukua pointi za msingi ambazo zitakusaidia katika kukuongoza. Mfano,
kuchukua takwimu, njia za kupata jibu na dokezo muhimu, maelezo mengine
unaachana nayo, kwani yatakuongezea mzigo wa kutafakari.
Njia
hii ya kuchambua mada au topiki itakusaidia kuhifadhi kumbukumbu,
hutakuwa mtu wa kusahau kwa sababu vitu ni vichache. Lakini pia utakuwa
umejiwekea msingi mkubwa wa kumudu kujikumbusha pale utakapokuwa na
hitaji la kufanya hivyo.
NNE: JIONGEZEE MAARIFA
Kile
ulichofundishwa kinaweza kuwa ni robo ya mada au somo husika; sasa ili
ujiongezee maarifa chukua muda wa kuchambua vile ulivyofundishwa kwa
kuvitafutia vyanzo vingine vya ufafanuzi. Inaweza kuwa ni kwa kusoma
vitabu, kuangalia kwenye intaneti au kutafuta mtu ambaye anauelewa juu
ya kile ulichofundishwa.
Faida
ya kufanya hivi ni kujishibisha maarifa. Mwalimu anaweza kuwa
amekufundisha jina la mgunduzi wa gari akaishia hapo, lakini unapozidi
kuchimba mwenyewe utajikuta unajua mguduzi huyo siyo tu alikuwa anaitwa
nani lakini ukoo wake, tabia zake au mji aliokuwa anaishi.
Katika
maarifa ambayo utajiongezea huenda ukakutana na kipengele ambacho
utakipenda na kukifanya simulizi na msisimko wa akili yako na hivyo kuwa
hodari katika kuelezea somo ulilojifunza na hivyo kujisogeza katika
ufaulu wa juu linapokuja suala la mitihani. Acha kutegemea maelezo na
notisi za mwalimu, jiongezee ufahamu.
TANO: JIWEKEE MSINGI WA KUJIZOEZA
Hata kama umeelewa kwa kiwango kikubwa usiache kujiwekea msingi wa kufanyia mazoezi yale uliyojifuza.
Unaweza
kujitungia mitihani na kufanya kila baada ya muda fulani au kuwa na
utaratibu wa kuzungumzia ulichojifunza mbele ya wenzako. Usione vibaya
kutumia muda wako kufundisha wengine kila unachoelewa kwani kadili
unavyofanya hivyo ndivyo unavyojijengea uwezo mkubwa wa kuelewa na
kukumbuka somo husika.
SITA: UMIZWA NA KUFELI
Kuna
baadhi ya wanafunzi ambao hata wakipata alama za chini kiasi gani
katika masomo yanayowashinda huwa hawaumizwi. Utasikia wanasema:
“Nashukuru hata kupata hizi alama 15 maana mimi nilitegemea ningepata
ziro kabisa.” Anafurahia kufeli. Usiwe mtu wa aina hii.
Kila
siku umizwa na kufeli kwa sababu kushindwa kwako katika ufaulu
kutakufanya usiwe daktari, injinia au mkemia taaluma ambazo unatamani
kuzipata. Mwanafunzi wangu; tambua kuwa hukuzaliwa uwe mtu wa chini
unatakiwa kuwa juu kama hao unaowaona na kuwahusudu. Jiamini.
Baada
ya kusema hayo usikose kusoma wiki ijayo mbinu mbadala za kufanya ikiwa
utatumia vitokezo hivi na kushindwa kukupatia unafuu katika masomo
unayoyaita magumu.
Nitafundisha
somo hili baada ya baadhi ya wanafunzi kunipigia simu na kunieleza kuwa
baadhi ya dokezo hizi wameshazifanya lakini hawajaona matokeo mazuri
katika masomo yao. Usikose kuungana nami ni muhimu sana kwako wewe
mwanafunzi wa ngazi yoyote ile!
itaendelea wiki ijayo